KAMATI ya Rufani ya Maadili ya Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) imewaadhibu walalamikiwa watano kati ya saba baada ya
kufanya mapitio (revision) kwa uamuzi wa Kamati ya Maadili kutokana na maombi
ya Sekretarieti, huku Richard Julius Rukambura akifungiwa miaka 20 kujihusisha
na mpira wa miguu.
Sekretarieti ya TFF iliwasilisha maombi ya mapitio
kwa Kamati ya Rufani ya Maadili ili kupata mwongozo kwa vile kulikuwapo
mkanganyiko kwenye uamuzi wa Kamati ya Maadili, hivyo kuiwia vigumu kwake
kuutekeleza.
Uamuzi huo wa mapitio umesomwa leo jioni (Oktoba 15
mwaka huu) mbele ya waandishi wa habari na wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa
na Makamu Mwenyekiti Victoria Makani.
Rukambura amefungiwa miaka 20 baada ya kupeleka
masuala ya mpira wa miguu katika mahakama za kawaida kinyume na Ibara ya 75 ya
Katiba ya TFF na kifungu cha 73(3)(b) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la
2013. Adhabu yake itamalizika Oktoba 15, 2033.
Kabla ya kutoa adhabu hiyo, Kamati imejiridhisha
kuwa Rukambura ni mwanafamilia wa TFF kwa vile aliwahi kuwa Mwenyekiti wa klabu
ya Pamba ya Mwanza, na fomu zake za kuomba uongozi TFF ziliidhinishwa na Chama
cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga. Vilevile ni ‘Leadership Aspirant’ kwa
mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii za TFF toleo la 2013.
Pia imesema kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya
Michezo kusajili Katiba ya TFF inayokataza masuala ya mpira wa miguu kwenda
katika mahakama za kawaida, na kutaja vyombo vya haki vitakavyoshughulikia
masuala hayo (judicial organs), Kamati ya Maadili ilikosea kutomtia hatiani
mlalamikiwa kwa kuegemea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye Shaffih Dauda, Kamati imebaini kuwa
mwanafamilia wa TFF kwani ni Mwenyekiti wa Bombom FC, fomu yake ya kuomba
uongozi ilipitishwa na klabu ya Simba na pia ameshakuwa kiongozi katika ngazi
mbalimbali ndani ya Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA), hivyo
yeye ni ‘Leadership Aspirant’ kwa mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii
za TFF toleo la 2013.
Hivyo Dauda amepatikana na kosa la kimaadili kwa
kutotekeleza maagizo rasmi ya TFF ya kutosambaza barua iliyotoka Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
Kamati ya Rufani ya Maadili imempa onyo kali na
faini ya sh. milioni moja anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu ambapo
akishindwa kufanya hivyo atafungiwa mwaka mmoja. Adhabu hiyo imetolewa kwa
mujibu wa kifungu cha 6(1)(a),(c) na (h) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la
2013.
Akilipa faini ataweza kuendelea na mchakato wa
kugombea nafasi ya uongozi aliyoomba.
Nazarius Kilungeja amepatikana na kosa la kimaadili
kwa mujibu wa kifungu cha 73(8)(a) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013,
kwani akijua kuwa ana adhabu ya kinidhamu ya kufungia miaka mitano na Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) iliyoanza 2009 alichukua fomu kuomba
uongozi TFF.
Hivyo, amefungiwa miaka mitatu, adhabu ambayo
itakwenda sambamba na ile ya RUREFA ambapo kifungo chake sasa kitamalizika
Oktoba 15, 2016.
Sekretarieti ya TFF imepewa onyo kali kwa kupokea
fomu yake ya kugombea na malipo wakati akiwa amefungiwa. Onyo hilo pia
limetolewa kwa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) Mkoa wa
Rukwa kwa kuidhinisha fomu yake ya kugombea.
Naye Wilfred Kidao Mzigama ambaye ni mjumbe wa
Mkutano Mkuu wa TFF amepatikana na kosa la kimaadili kwa kuwa na nyaraka la
Kamati ya Utendaji bila kibali na kukiuka taratibu za kuwasilisha malalamiko
kwa mujibu wa Ibara ya 12(2) na Ibara ya 50(1) na (5) ya Katiba ya TFF.
Amepigwa faini ya sh. milioni moja anayotakiwa kuilipa
ndani ya siku tatu ambapo akishindwa atafungiwa mwaka mmoja. Akitekeleza adhabu
hiyo ataweza kuendelea na mchakato wa kugombea uongozi kwa nafasi aliyoomba.
Vilevile Kamati hiyo imetoa onyo kali kwa
Sekretarieti ya TFF na wajumbe wa Kamati ya Utendaji kwa kushindwa kudhibiti
nyaraka muhimu za vyombo vyao.
Pia Kamati ya Rufani ya Maadili imempata na kosa la
kimaadili Kamwanga Tambwe kwa mujibu wa kifungu cha 73(8) cha Kanuni za Maadili
za TFF toleo la 2013, kwa kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wakati ana adhabu
ya kinidhamu inayomalizika 2014.
Hivyo, amepewa adhabu ya kufungiwa miaka mitatu
ambayo itakwenda sambamba na ile ya kinidhamu na kumalizika Oktoba 15, 2016.
Pia Sekretarieti ya TFF, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma (FARU) na
Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) Mkoa wa Ruvuma wamepewa
onyo kali kwa kupokea na kuidhinisha fomu zake za kugombea uongozi wakati
akitumikia adhabu ya kufungiwa.
Kamati ya Rufani ya Maadili imewakuta kutokuwa na
hatia ya makosa ya maadili kama ilivyobaini Kamati ya Maadili walalamikiwa
Riziki Juma Majala na Omar Isack Abdulkadir, hivyo wana haki ya kugombea
uongozi kwa kufuata Katiba na Kanuni za TFF.
Kwa mujibu wa kifungu cha 74(4) cha Kanuni za
Maadili za TFF toleo la 2013, uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Maadili hauna fursa
ya rufani wala marekebisho kutoka chombo kingine chochote isipokuwa FIFA na
Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).
0 comments