YANGA na Simba kwa pamoja leo zinashuka katika
viwanja viwili tofauti kupambana na Rhino Rangers na Coastal Union katika
muendelezo wa Ligi Kuu ya Bara.
Yanga ambayo ni mabingwa watetezi wenyewe watakuwa
jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, kuvaana na Rhino ya Tabora
inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JW).
Kocha msaidizi wa Yanga, Fred Minziro amesema vijana
wake wamefuta makosa na sasa wapo tayari kuikabiri Rhino Rangers leo.
“Kikosi kipo sawa kupambana na Rhino hapo kesho
(leo), kama ni makosa tumeshayafanyia kazi na nadhani tutafanya vizuri zaidi
katika mchezo huu na kilichobaki sasa ni muda kufika tuweze kuingia uwanjani,”
anasema Minziro.
Yanga ilianza mazoezi juzi Jumatatu asubuhi kwenye
Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyora jijini Dar es Salaam baada ya Jumapili
kutoka sare na Simba ya mabao 3-3 na Simba kwenye Uwanja wa Taifa.
Hadi sasa Yanga ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 16
katika michezo 9. Rhino yenyewe ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 7 katika
michezo 9.
NAKO mjini Tanga, Simba inashuka dimbani leo mchana
kupambana na Coastal Union ya mjini humo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya
kutwaa ubingwa.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekile Kamwaga ameuambia mtandao
huu kwamba, kikosi cha Simba kiliwasili salama Jumatatu jijini Tanga tayari kwa
mchezo huo wa leo na wachezaji Henry Joseph, Haruna Chanongo na Abdulhalim
Humud hawapo katika kikosi hicho.
“Timu imefika salama Tanga tangu Jumatatu mchana na
hali ya kikosi kizima ni nzuri kinachosubiriwa sasa ni muda kufika ili tuweze
kutazama pambano hili safi na la kuvutia kwetu sote, kwani Coastal ni timu
nzuri ambayo ina wachezaji kadhaa ambao wamewahi kuwika na klabu mbalimbali za
hapa nchini.
“Sisi kama Simba tunaamini tuna timu nzuri ambayo
inaweza kupambana na timu yoyote na kutwaa ubingwa hivyo wakazi wa Tanga na
miji ya jirani wajitokeze kwa wingi uwanjani kutazama pambano hili la kuvutia,”
anasema Kamwaga.
Naye Mwenyekiti wa Coastal, Ahmed Aurora amesema
kikosi cha timu yake kimejiandaa vya kutosha na hakuna tatizo lolote
linaloikabiri timu yake kuelekea mchezo wa leo dhidi ya Simba.
“Sisi tupo vizuri kabisa tunaisubiri Simba kwa hamu
kubwa kuweza kupambana nao kwani tumejiandaa vizuri chini ya kocha wetu Joseph
Lazaro ambaye amejiunga nasi hivi karibuni akichukua nafasi ya Ahmed Morocco.
“Tuna wachezaji wengi wazuri ambao wamewahi kutamba
na timu kubwa za Simba, Yanga na Azam, tunachohitaji sisi ni kufanya vizuri
kwenye uwanja wetu wa nyumbani,” anasema Aurora.
0 comments