MWENYEKITI wa Chama cha Waandishi wa Habari za
Michezo nchini, Juma Pinto amefunguka na kueleza sera na mikakati yake
atakapoingia kwenye Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Uchaguzi huo wa TFF unatarajia kufanyika Jumapili ya
Oktoba 27, Pinto anagombea nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda
ya Pwani na Morogoro.
Pinto aliuambia mtandao huu kuwa, nimeamua kugombea
nafasi hiyo ili kuleta mabadiliko ya
kweli na kuleta fikra endelevu katika soka la Tanzania.
Naamini kabisa nikichaguliwa katika nafasi hiyo kwa
kushirikiana na viongozi wenzangu tutaleta mafanikio zaidi na hususani kupokea
kijiti kwa viongozi wenzetu waliotangulia ambao wameweka mfumo mzuri wa utawala
bora ndani ya shirikisho.
Ili mafanikio yaweze kupatikane ni lazima tuweke
mpango endelevu kwa kuwekeza zaidi katika soka la vijana, kuandaa kozi ,warsha
na makongamano yatakayotupa dira nzuri ya kukuza na kuwaendeleza vijana na
mchezo wenyewe wa soka.
Kikubwa ambacho nitahakikisha ntalisimia kidedea ni
kuendeleza vipaji vya wachezaji chipukizi, kuandaa makocha, waamuzi chipukizi
na upatikanaji wa vifaa vya michezo ikiwemo kuhakikisha viwanja vya michezo
havitumiki kwa matumizi mengine na hivi vilivyopo viweze kuboreshwa zaidi.
Lingine ni kuhakikisha mikoa yote nchini inapata
haki sawa katika kugawiwa rasilimali zinazopatikana kutoka kwa wadhamini na
Shirikisho la kandanda duniani (FIFA) na kuhakikisha mfumo wa kutumia tiketi za
elektroniki unaanza kutumika mara moja.
Mfumo huo utasaidia kumaliza tuhuma za ubadhirifu wa
mapato ya milangoni katika mechi mbalimbali zinazofanyika nchini katika viwanja
mbalimbali.Zinapopatikana pesa kwa wingi ndio tutakapoweza kutumia fursa hiyo
kufanya maendeleo ya mpira wa miguu.
Nafahamu majukumu mazito ambayo yanatakiwa kutekelezwa
na kamati ya utendaji na nikiwa kama mjumbe nafahamu nchi yetu ambayo imekuwa
ikikumbwa na changamoto mbalimbali katika uendelezaji wa michezo hasa mchezo wa
soka.
Kwa miaka 13 iliyokaa Uingereza niliweza kupata
nafasi ya kufanya kazi (Part time) pale
BBC Swahili kwa kweli niliweza kupata ufahamu
wa hali ya juu sana kuhusu mpira wa miguu na kufanya utafiti wa kina
katika michezo ikiwa ni pamoja na wachezaji wake, viwanja, kanuni na mbinu
mbalimbali.
Lakini mwaka 1999 niliweza kupata semina ya siku 45
nchini Brazili juu ya uongozi wa mpira
wa miguu (Football Administration), hatua ambayo ilinipata weledi mkubwa sana katika uongozi wa mchezo wa mpira wa
miguu.
Nina uhakika kwa hayo yote niliyoyapata kabla na
baada ya kuondoka nchini, yameweza kunipa mwanga sahihi wapi tunapotakiwa
kwenda, lakini pia kupata fursa ya kuweza kutumia uzoefu wangu na hiki
nilichokipata kuweza kutumia ndani ya TFF.
Hivyo nimeamua kuingia TFF ili kutumia uzoefu wangu
katika kuleta mabadiliko ya kweli, pamoja na kuwa mchezaji wa timu ya Pan
African mwaka 1993, pia na mchezaji wa timu ya Taifa ya Vijana mwaka 1994.
Lakini kwa hivi sasa ni mjumbe wa Baraza la Michezo
la Taifa (BMT), Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Chama Cha soka mkoa wa Pwani,
Mjumbe wa kamati ya masoko ya TFF na Mwenyekiti wa Chaa Cha Waandishi wa Habari
za Michezo (TASWA).
0 comments