Miss Utalii Tanzania 2013, Hadija Mswaga
(kushoto) akiingia kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini
Dar es Salaam, kuelekea Equatorial Guinea kuiwakilisha Tanzania katika
mashindano ya Dunia ya Miss Tourism World 2013, pembeni ni mshindi wa tatu,
Teresia Kimolo aliyemsindikiza.
BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata), limempa karipio kali Mwenyekiti wa shindano la Miss Utalii, Gideon Chipungahelo kwa kosa la kudhalilisha baadhi ya washiriki na malalamiko kufanyiwa kazi na Baraza hilo.
Karipio hilo lilitolewa baada ya Basata kupitia
tathmini iliyohusisha vipande vya matukio yaliyorekodiwa (clips) na kujionea
namna wasichana wanavyofanyiwa vitendo vya udhalilishaji na Chipungahelo kwa
kipindi cha kambi ya miezi mitatu.
Katika hafla ya upitiaji wa clips hizo uliofanyika
mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Basata, Ilala, jijini Dar es Salaam mbele ya
Chipungahelo, ilionekana wazi wasichana kukosa uangalizi walipokuwa kambini,
hivyo kuwepo kwa matukio mbalimbali yasiyofaa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa kitengo cha
Sanaa wa Basata, Nsao Shaluwa alisema baada ya kupata malalamiko kuwa wasichana
wanafanyiwa mambo yasiyofaa wakiwa kambini, waliamua kuutafuta ukweli na
kujiridhisha shindano hilo lina ukakasi mwingi.
Alisema baada ya kukusanya baadhi ya matukio katika
kuthibitisha hali halisi iliyopo kwenye shindano hilo, watapeleka vielelezo kwa
Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana Michezo na Utamaduni ili Chipungahelo
ajadiliwe kwa kosa la kudhalilisha warembo wa shindano hilo.
Alisema kwa kukosa matroni, yaelezwa warembo
walikuwa wakizurula kutwa nzima hadi usiku kwenye gari huku kukiwa hakuna
ratiba ya chakula ya kueleweka huku wakifanyishwa mazoezi muda mrefu.
Mbali ya muda mrefu kuanzia saa 2 usiku hadi 9, pia
walikuwa wakivaa viatu virefu, hivyo miguu kuvimba na wakati mwingine walikuwa
wakichapwa makofi na kulazimishwa mapenzi.
Aidha, Chipungahelo anakabiliwa na shutuma ya
kuwaweka mabinti washiriki kwa muda wa miezi mitatu tofauti na alivyoeleza
Basata kuwa kambi ni ya wiki tatu.
Zaidi ya hapo, Chipungahelo alishindwa kutoa zawadi
kwa washindi wala kifuta jasho kwa washiriki wengine huku mshindi wa mwaka
2013, akidaiwa kubebwa kwa hila.
Shaluwa alisema baada ya malalamiko hayo kufikishwa
kwao, waliamua kunyatia katika kambi yake iliyokuwa na warembo saba ambayo pia
Chipungahelo aliwaficha.
Baada ya kuwahoji washiriki, walikiri kwamba
walikuwa wakilala warembo saba, wengine watano katika chumba kimoja na wengine
wakilala chini huku wakila mlo mmoja tena katika muda usiofaa.
“Tulikuwa tukifanyishwa mazoezi kuanzia saa mbili
usiku hadi saa tisa, tuna njaa na tulipolalamika, baba alitutukana matusi ya
nguoni na kukashifu tupu zetu,” alisema mmoja wa warembo katika CD ya Basata.
Shaluwa anasema walipofika Ikondolelo ambako
kulikuwa na kambi ya awali, walizungumza na warembo hao, lakini wakishindwa
kusema ukweli mbele ya Chipungahelo.
Alisema walipowapa karatasi kuandika kero zao, kila
mtu aliandika jina na kusaini ambapo walieleza mengi yaliyorekodiwa na wadau
kuoneshwa mwishoni mwa wiki mbele ya mwanasheria Ashura Mzava kutoka TAWLA.
Mzava alisema wazi kwa madudu yaliyopo kwenye
shindano hilo, Chipungahelo anapaswa kushtakiwa kwa udhalilishaji.
Kashfa nyingine ni kitendo cha Chipungahelo kutumia
kiasi cha Sh. 200,000 ambazo zilitolewa na Mkuu wa Wilaya Tanga Mjini, Halima
Dendego ili washiriki waende saloon kabla ya fainali.
“Baba ametunyanyasa sana hadi, ametumia pesa
tuliyopewa na mama Halima Dendego, lakini hapohapo amekuwa akimpendelea
mshiriki mwenzetu (jina tunalo), kwa vile alikuwa na uhusiano naye wa
kimapenzi,” alisema mmoja wa washiriki na kuongeza.
“Hata siku ile ya fainali, alipokuja mpambaji kutoka
Sofia Record, alimwita na kumvalisha nguo nzuri pamoja na kumpamba tofauti na
alivyovalishwa washiriki wengine.”
Wakati huohuo Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa kutoka
Wizarani, Leah Kihimbi alisema atalifikisha kwa usahihi suala hilo katika ngazi
ya juu akimtaka Chipungahelo ajitayarishe kwa maamuzi yoyote.
Mshiriki pekee wa Miss Utalii 2013 aliyefika kwenye
tahmini hiyo, ni Glory John aliyesema wazi shutuma zote zilizoelezwa na wenzake
dhidi ya Chipungahelo ni kweli.
“Tulipokuwa tunakwenda Mikumi , tulilala Morogoro,
Baba (Chipungahelo) aliniita akaniambia nipande juu katika chumba kimojawapo,
nilipokwenda na kufungua mlango, nikakutana na moshi wa ajabu nikashindwa
kuvumilia nikatoka.
Akanifuata akinitaka nirudi chmbani mle, nikagoma,
nilipowaeleza wenzangu, walinieleza nilielekea kunaswa kwenye mtego wake,”
alisema Glory.
Naye Katibu Mtendaji BASATA, Godfrey Mngereza
alisema, hilo ni suala nyeti linalogusa jinsia ya kike, hivyo ni hatari kwa
ustawi wa jamii.
Kupitia tathmini hiyo ya aina yake, Basata
itachunguza mazingira ya ushindi wa Miss Utalii mwaka 2013, ikibainika
hakustahili, atavuliwa taji hilo ili iwe fundisho.
“Tabia hizi chafu zinatuchafua hata sisi BASATA
tunaonekana hatufanyi kazi sasa ndio tutaanza na Miss Utalii na ikibidi kusiwe
na shindano la aina yeyote kama mambo yenyewe ni kudhalilishana,” alisema
Mngereza.
Wadau wengine waliohudhuria tathmini hiyo ni kutoka
TAMWA, TAWLA, TGNP, THAWE, Polisi Jamii, Polisi kutoka kituo cha Pangani Ilala,
Dar es Salaam, Shirikisho la Sanaa na Ufundi, Binti Leo na wengineo.
Shaluwa alisema suala hilo litapelekwa ngazi za juu
na vielelezo kuonesha wasichana wakieleza yanayotokea kambini pamoja na maoni
ya wadau yaliyorekodiwa.
Akizungumzia tuhuma dhidi yake, Chipungahelo alisema
ni majungu yaliyopikwa na maadui zake ambao walimpandikizia makahaba kwa lengo
la kuchafua taswira ya shindano hilo ili kummaliza, lakini aliomba radhi kwa
dosari na mapungufu yaliyojitokeza na kuahidi kuwa hazitajirudia tena.
0 comments