RAIS mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania,
Jamal Malinzi ameendelea kupokea salamu za pongezi baada ya kushinda wadhifa
huo katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 mwaka huu.
Salamu nyingine za zimetoka kwa Rais wa Shirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Sepp Blatter ambapo amempongeza Malinzi
kwa kuchaguliwa na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake ya kuongoza
mchezo huo nchini.
Blatter amesema ana uhakika ufahamu wake na uwezo
wake katika uongozi ni muhimu katika kuimarisha maendeleo ya mpira wa miguu
nchini, na kuongeza kuwa milango ya FIFA iko wazi wakati wowote anapotaka
kujadili masuala yanayohusu mchezo huo.
“Nakutakia wewe na kamati mpya ya Utendaji iliyochaguliwa
kila la kheri, nguvu, na kila aina ya mafanikio kwa changamoto zilizo mbele
yenu,” amesema Rais Blatter katika salamu zake.
Wengine waliomtumia Rais Malinzi salamu za pongezi
ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), Sam Nyamweya, Rais wa
Heshima wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Lawrence
Mulindwa, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) na Mwenyekiti wa Chama
cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Arumeru (ADFA), Peter Temu.
0 comments