UJENZI wa Uwanja utakaochezewa mechi za fainali za Kombe
la Dunia la 2014 nchini Brazil zimesimamishwa baada ya jaji wa mahakama kusema
kuna wasiwasi kuhusu usalama.
Uwanja huo wa Arena da Baixada katika jiji la
Curitiba ulipangiwa kuchezwa mechi nne za kombe la dunia. Ukarabati wa uwanja
huo ulikwishacheleweshwa kwa kipindi kadhaa.
Jaji Lorena Colnago alisema maisha ya wafanyakazi
yanahatarishwa kutokana na hali ya kuzorota kwa ujenzi huo. Akiongeza kusema kuna
hatari ya kuzikwa, kukanyagwa na magari na hata kudondoka kutoka kuta za juu za
uwanja huo.
Aliamrisha ukaguzi mpya ufanywe kabla ya kuanza tena
shughuli za ujenzi. Akiongeza kusema kumegunduliwa kasoro nyingi katika ujenzi
huo.
Taarifa hizo zinakuja wiki moja tu baada ya
uchunguzi kufichua kwamba wafanyakazi walioajiriwa katika ujenzi wa mradi
mwingine wa kombe la dunia walikabiliwa na hali ya kitumwa.
Wachunguzi hao walisema pia kwamba zaidi ya wafanyakazi
100 walioajiriwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sao Paulo wanaishi
katika hali duni karibu na uwanja huo.
Mnamo mwezi wa Agosti, Waziri wa Michezo, Aldo
Rebelo alisema ana wasiwasi jinsi ujenzi ulivyochelewa katika viwanja vitano
vya michuano ya kombe la dunia mwakani.
Baada ya ziara yake nchini Brazil, Katibu Mkuu wa
FIFA, Jerome Valcke, alisema viwanja vyote lazima viwe tayari ifikapo mwezi
Desemba na kuonya hatavumilia tena kuchelewesha ujenzi na hakuna 'mpango
mbadala'.
Michuano ya kombe la dunia imepangwa katika viwanja
12 nchini kote Brazil.
0 comments