UAMUZI KAMATI YA MAADILI KUFANYIWA MAPITIO
Shirikisho liko kwenye hatua za mwisho za mchakato
wa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 26/27 Oktoba 2013 hapa jijini Dar
es salaam.
Hivi sasa, wagombea wanasubiri vyombo vya juu vya
uamuzi kwa ajili ya kutoa uamuzi wa mwisho kabla ya kuanza kampeni na hatimaye
uchaguzi.
Hata hivyo, baada ya Kamati ya Maadili kufanya
uamuzi dhidi ya kesi nane zilizowasilishwa mbele yake, Sekretarieti imeona
kuwepo kwa ukakasi katika utekelezaji wa uamuzi huo kutokana na ukweli kuwa
kuna baadhi ya mambo yanaonekana kuwa na ugumu katika kuyatekeleza.
Sekretarieti si chombo chenya mamlaka ya kutafsiri
uamuzi wa vyombo huru vya Shirikisho, kazi yake kubwa ni kupokea uamuzi na
kuutekeleza, hivyo kwa kuwa kuna ukakasi huo imeamua kuwasilisha uamuzi huo
kwenye Kamati ya Rufani ya Maadili kwa ajili ya kuufanyia mapitio (revision) na
pia kutoa mwongozo kabla ya kurejesha uamuzi huo kwenye Kamati ya Uchaguzi kwa ajili
ya kuendelea na mchakato.
Sekretarieti imefanya hivyo kwa lengo la kusaidia
wagombea ambao wengi wanaonekana kuwa njia panda baada ya kupokea uamuzi wa
Kamati ya Maadili na kuiuliza Sekretarieti kuwa inakuwaje Kamati ya Maadili
iwaone hawana hatia, lakini hapo hapo ikubaliane na uamuzi wa kuwaengua, jambo
ambalo kwa kweli limetufanya tukose majibu sahihi na hivyo kuamua kuomba
revision na mwongozo.
Pia mwongozo utakaotolewa na Kamati ya Rufani ya
Maadili utasaidia kuweka mwelekeo mzuri wa masuala ya Maadili katika siku
zijazo.
Miongoni mwa mambo yanayoonekana kuwa na ukakasi ni
kuwaona watu wote ambao kesi zao ziliwasilishwa kwenye Kamati ya Maadili hawana
hatia, lakini hapo hapo kukubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi wa
kuwaengua baadhi yao kwa sababu za kinidhamu ikisema haiwezi kuwahukumu mara
mbili kwa kuwa wameshaadhibiwa kwa kuenguliwa kwenye uchaguzi.
Ili haki itendeke na ionekane inatendeka,
Sekretarieti imeona ni vizuri masuala hayo yakafanyiwa revision (mapitio) na
kutolewa mwongozo ili kuondoa ukakasi uliojitokeza miongoni mwa wagombea,
Shirikisho na wadau na hivyo kujenga hisia kuwa kuna mbinu zimefanyika dhidi ya
baadhi ya wagombea.
Uamuzi huu haumaaniishi kuwa Sekretarieti inapingana
na uamuzi wa Kamati ya Maadili, bali ni utaratibu wa Sekretarieti kuomba
ufafanuzi au mwongozo kutoka vyombo husika pindi inapotokea ukakasi katika
utekelezaji wa uamuzi wa vyombo vya uamuzi vya Shirikisho.
Sekretarieti imeshamwandikia Mwenyekiti wa Kamati ya
Rufani za Maadili ili aitishe kikao kwa manajiri ya kufanya mapitio na kutoa
mwongozo ambao utasaidia Shirikisho kuendelea na uchaguzi bila ya ukakasi.
SERIKALI, TAASISI ZAOMBWA KUISAIDIA U20 WANAWAKE
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
limeiomba Serikali, taasisi na kampuni mbalimbali kuisaidia timu ya Taifa ya
mpira wa miguu ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 inayojiwinda
kwa mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Msumbiji.
Timu hiyo hivi sasa iko kambini Mlandizi mkoani
Pwani chini ya Kocha Rogasian Kaijage kujiandaa kwa mechi hiyo ya kwanza ya
raundi ya kwanza itakayochezwa Oktoba 26 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu ya Wanawake
ya TFF, Lina Kessy amesema hiki ndio kipindi muafaka cha kuisaidia timu hiyo
ili iweze kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Ameitaka jamii kujitokeza kuisaidia timu hiyo ambayo
haina mdhamini wala mfadhili, kwani timu za Taifa ni za Watanzania badala ya
kusubiri ifanye vibaya na kusema ni kichwa cha mwendawazimu.
Kessy ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa
Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA), ameishukuru kambi ya JKT Ruvu kwa kutoa
fursa ya kambi kwani timu hiyo hailipii malazi badala yake inalipia huduma
nyingine inazopata hapo.
Vilevile amewashukuru wadau mbalimbali ambao
wamekuwa wakijitolea kutokana na ukweli kuwa tangu kuanza mashindano ya mpira
wa miguu wa wanawake kumekuwepo uungwaji mkono mkubwa.
“Shukrani za kipekee kwa wazazi kukubali watoto wao
wachezee timu ya Taifa, kwani wengi bado wanasoma na wapo chini ya uangalizi wa
wazazi. Pia tunawaomba wazazi wajitokeze mazoezini ili kuwajenga kisaikolojia
wachezaji wetu,” amesema.
Fainali za Dunia za U 20 kwa wanawake zitafanyika
mwakani nchini Canada. Iwapo Tanzania itaitoa Msumbiji katika raundi hiyo,
raundi inayofuata itacheza na mshindi kati ya Botswana na Zimbabwe.
WASHABIKI WENYE SILAHA MARUFUKU VIWANJANI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia
Jeshi la Polisi kuanzia sasa halitashikilia silaha za washabiki, na badala yake
litawazuia kabisa kuingia viwanjani wakati wa mechi.
Jeshi la Polisi limekuwa likihifadhi silaha za
washabiki wanaokwenda viwanjani, na baadaye kuwarejeshea baada ya mechi
kumalizika kwa vile Kanuni za Usalama Viwanjani za Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA) zinakataza silaha viwanjani.
Wikiendi iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, Jeshi la Polisi lilikamata bastola 17 katika upekuzi wa washabiki
waliokwenda kushuhudia mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting na ile kati ya JKT
Ruvu na Simba. Wote waliokutwa na silaha hizo walikuwa na leseni za kuzimiliki.
Hivyo, kwa washabiki wanaomiliki silaha
hatawaruhusiwa kabisa kuingia viwanjani, na badala yake tunawashauri
kuzihifadhi huko wanakotoka kabla ya kufika viwanjani.
Pia tunatoa mwito kwa shabiki ambaye atamuona
mwenzake akiwa na silaha uwanja kutoa taarifa kwa mamlaka husika likiwemo Jeshi
la Polisi ili aweze kuchukuliwa hatua.
SIMBA KUIVAA RUVU SHOOTING VPL
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania
ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya saba kesho (Oktoba 5 mwaka
huu) kwa mechi nne ambapo Ruvu Shooting
itakuwa mwenyeji wa vinara Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na
mwamuzi Mohamed Theofil kutoka Morogoro kuanzia saa 10 kamili jioni vitakuwa
sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani
kuanzia saa 4 asubuhi.
Mechi nyingine za kesho ni JKT Ruvu itakayoumana na
Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam huku Coastal Union
ikiwa mwenyeji wa Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid
jijini Arusha ndiyo utakaotoa fursa kwa timu za Oljoro JKT na Mbeya City
kuoneshana ujuzi katika kusaka pointi tatu.
Ligi hiyo itaendelea Jumapili (Oktoba 6 mwaka huu)
kwa mechi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
wakati Mgambo Shooting itaialika Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga.
FDL KUTIMUA VUMBI VIWANJA KUMI
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwania tiketi za
kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao (2014/2015) inaendelea wikiendi
hii (Jumamosi na Jumapili) kwa kuzikutanisha timu 20 zitakazopambana katika
viwanja kumi tofauti.
Jumamosi kutakuwa na mechi kati ya Green Warriors na
Friends Rangers (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi), Kimondo na Burkina Faso (Uwanja
wa CCM Vwawa, Mbozi), Mlale JKT na Mkamba Rangers (Uwanja wa Majimaji, Songea)
na Kurugenzi dhidi ya Polisi Morogoro (Uwanja wa Wambi, Mafinga).
Polisi Dodoma na Stand United (Uwanja wa Jamhuri,
Dodoma), Toto Africans na JKT Kanembwa (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Mwadui
na Polisi Mara (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga) na Polisi Tabora na Pamba
(Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
Keshokutwa (Jumapili) kutakuwa na mechi kati ya
African Lyon na Transit Camp (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi) na Villa Squad
dhidi ya Polisi Dar es Salaam (Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam).
0 comments