BENDI ya taarabu ya Mashauzi Classic kesho
(Jumatano) itatambulisha nyimbo zao mpya kwenye onyesho maalum ya kusherehekea
sikukuu ya Idd el Hajj katika ukumbi wa Dar West Park, Tabata.
Onyesho hilo ambalo linajulikana kama ‘Usiku wa Isha
Mashauzi’, imeandaliwa na Keen Arts na
Bob Entertainment chini ya udhamini wa kinywaji cha Konyagi, Straika,
Kwetu Mbambabay na Saluti5.
Mratibu wa onyesho hilo, Joseph Kapinga amesema kuwa
onyesho litakuwa la kipekee na maalum kwa kusherehekea sikukuu ya Idd El Hajj.
Amesema katika onyesho hilo, Mashauzi atatambulisha
albamu yake mpya ijulikanayo kama “Asiyekujua Hakuthamini” ambayo ina nyimbo
kama “Mimi Bonge la Bwana,” utunzi wake Hashim Said, “Ropokeni Yanayoyahusu” (
Saida Ramadhani) na “Haya ni Mapenzi Tu” (Zubeda Malik). Zawadi mbalimabli
zitatolewa kwa mashabiki wa bendi hiyo inayojulikana kama Wakali wa Kujiachia.
“Tumeandaa zawadi mbalimbali kwa mashabiki wetu. Pia
bendi ya Mashauzi Classic watatumia onyesho hilo kutambulisha nyimbo zao mpya,”
Kapinga alisema.
“Mashauzi Classic watapiga albamu zao zote.
Matumaini yetu ni kuwa watu watapata burudani ya kutosha kuliko siku zingine
zote,” alisema Kapinga.
Nyimbo zingine zitakazopigwa ni “Viwavijeshi” (Issa Ramadhani), “Sitasahau
Yaliyonikuta” (Abdul Malik), “La Mungu Halima Mwamuzi” (Zubeda Malik) na
“Sijamuona Kati Yenu” (Rukia Juma).
Naye mkurugenzi wa bendi hiyo, Isha Mashauzi,
alisema kuwa onyesho la Da West litakuwa la kihistoria na kutaka watu
wajitokeze kwa wingi ili historia isiwapite. “Kwa kweli bendi iko fiti,”
alisema Mashauzi.
0 comments