UCHAGUZI wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPL Board)
utafanyika Oktoba 25 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee
Tower.
Kwa mujibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wajumbe wanaounda Mkutano wa Uchaguzi ni
wenyeviti kutoka klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na 14 wa klabu za
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).
Wagombea kwenye uchaguzi huo ni Hamad Yahya Juma
(Mwenyekiti), Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti) wakati wanaoumba
ujumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Khatib Omari Mwindadi na Kazimoto Muzo.
Wakati huo huo, Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mjumbe wa Bodi ya klabu ya
Ashanti United, Jimmy Mhango kilichotokea jana (Oktoba 21 mwaka huu).
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu
kwani Mhango aliutumikia mpira wa miguu kwa muda mrefu, tangu akiwa mchezaji,
kocha na baadaye kiongozi.
Kabla ya kuingia kwenye Bodi ya Ashanti United, enzi
za uchezaji wake alichezea timu za Mapinduzi ya Dodoma, Ushirika ya Moshi na Pan
African ya Dar es Salaam. Pia aliwahi kuwa Kocha Mkuu wa Ashanti United.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Mhango,
klabu ya Ashanti United na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam
(DRFA), na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha
msiba huo mzito.
Maziko yamefanyika leo mchana katika makaburi ya
Abeid (Mchikichini) Dar es Salaam. Mungu aiweke roho ya marehemu Mhango mahali
pema peponi. Amina
0 comments