MALKIA wa Uingereza ameanzisha rasmi mbio za
kupokezana rungu la michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika mjini Glasgow
Scotland mwaka 2014.
Rungu hiyo ina risala aliyoiandika kwa mkono Malkia
kwa Jumuiya ya Madola itakayosafirishwa katika mataifa na maeneo yote 70
yatakayoshiriki katika michezo hiyo katika kipindi cha siku 288 zijazo.
Rungu hilo litasafirishwa kwanza hadi Scotland mnamo
siku ya Alhamisi kabla ya kuelekea India kwa kituo chake cha kwanza cha
kimataifa Oktoba 11.
Safari ya rungu hilo itamalizika wakati wa sherehe
za ufunguzi za michezo hiyo Julai 2014, ambapo Malkia ataisoma risala iliyomo
ndani yake.
Katika sherehe za uzinduzi ziliofanyika katika kasri
ya Malkia mjini London, Rais wa Shirikisho la michezo ya Jumuiya ya Madola,
Prince Imran wa Malaysia, amesema mbio za rungu hilo lina ujumbe mzito wenye
maana.
"Mbio za kupokezana rungu hilo zinawaunganisha
raia billioni 2 wa Jumuiya ya Madola katika kusherehekea michezo, kabila
tofauti na amani na kudumisha urafiki na uhusiano wetu" alisema Imran.
Baada ya hotuba Malkia alitumbukiza waraka wenye
risala yake ndani ya rungu hilo na kisha kufungwa kwa safari yake ya kilometa
190,000 kupitia mabara ya Asia, Oceania, Afrika, Amerika za Kaskazini na Kusini
na Caribbean.
Wa kwanza kukimbiza rungu hilo alikua Alan Wells, mwanariadha
wa mbio fupi wa Scotland aliyeshinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 100
za Olimpiki ya 1980 mjini Moscow.
0 comments