MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto’o
amekubali kubadili maamuzi yake ya kustaafu kucheza soka la kimataifa baada ya
kuomba na Rais wa nchi hiyo, Paul Biya.
Eto’o anayeichezea timu ya Chelsea kwa sasa,
aliwatangazia wachezaji wenzake mwezi uliopita kuwa hataichezea tena timu hiyo
lakini Rais Biya amemuomba nyota huyo kubadiliusha maamuzi yake na kuitumikia
tena nchi yake.
Baada ya rais huyo kuzungumza na Eto'o, amekubali kuichezea
Cameroon kwa mara nyingine na sasa atakwenda Ufaransa kujiunga na wachezaji
wenzake kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Tunisia utakaochezwa Jumapili ya
Oktoba 13 kuwania kufufuzu fainali za Kombe la Dunia Brazil mwaka 2014.
“Unaweza kuwa na matatizo popote pale utakapokuwepo
duniani, lakini cha muhimu kuangalia jinsi ya kuyamaliza,” alisema Eto’o. “Sasa
nimeamua kurudi tena na nitajiunga na wachezaji wenzangu katika mchezo na
Tunisia na kurudi kwangu kutakuwa na matokeo mazuri.”
Licha kuwepo ripoti za Eto’o kuacha kucheza soka,
kocha wa timu ya Cameroon Volker Finke alimteua mshambuliaji huyo katika kikosi
kitakachoivaa Tunisia.
Eto'o amekuwa na uhusiano tete na maafisa wa soka
nchini Cameroon katika siku za nyuma ikiwemo hata kuongoza timu ya taifa kwenye
mgomo uliosambaratisha mechi ya kirafiki dhidi ya Algeria.
Eto’o aliadhibiwa kwa kupigwa marufuku kucheza mechi
15 ingawa baada ya kukata rufaa alipunguziwa adhabu hadi mechi 8
Hata baada ya adhabu yake kumalizika alikataa
kuichezea Cameroon kwa miezi kadhaa. Hii siyo mara ya kwanza kwa Rais Biya
kuingilia kati na kumzuia mchezaji kujiuzulu kutoka katika majukumu ya kitaifa.
0 comments